WIZARA ya Maliasili na Utalii, imeanza mchakato wa kuandaa mfuko
wa kulinda Mlima Kilimanjaro dhidi ya majanga ya moto pamoja na
uandaaji wa rasimu ya mfumo maalumu unaoshirikisha kada mbalimbali
kwenye ulinzi wa hifadhi za taifa.
Wizara imefikia hatua hiyo kutokana na kuwapo kwa matukio ya moto ya
mara kwa mara katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, yanayodaiwa
kusababishwa na shughuli za kurina asali ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza na uongozi wa hifadhi ya taifa ya Mlima Kilimanjaro na
vikosi vya askari mgambo na askari polisi wa Chuo cha Polisi Moshi
walioshiriki zoezi la kuzima moto katika mlima huo, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema mfumo huo utakuwa
shirikishi.
“Mfumo huu utakuwa ni shirikishi na utawahusisha wananchi katika
vijiji vinavyozunguka hifadhi na pia utazihusisha halmashauri za wilaya.
Sasa hili liko kwenye mchakato na sasa tunaandaa rasimu ya uendeshaji
wa mfumo huo,” alisema Nyalandu.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa nchi za kusini mwa
Afrika (SADC), ambazo zinaingizwa kwenye mfumo unaoanzishwa wa kutambua
moto kwa njia ya satellite, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuwezesha wakuu
wa hifadhi kuweza kubaini matukio hayo kabla hayajaleta maafa makubwa
zaidi.
Katika hatua nyingine, Nyalandu alitoa agizo la kuzuia utoaji wa
vibali vya kuvuna kuni na urinaji asali ndani ya hifadhi ya Mlima
Kilimanjaro na badala yake vitatolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA).
Katika agizo hilo, Nyalandu alisema uamuzi huo unatokana na matokeo ya
utafiti wa majanga ya moto ndani ya hifadhi hiyo kuonyesha kuwa chanzo
kikuu ni urinaji wa asali au uvunaji wa kuni unaofanywa na baadhi ya
wananchi waishio vijiji jirani.
Nyalandu alisema amri hiyo ya serikali inapaswa kuheshimiwa na kila
mmoja, na akaonya hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaobainika
kuikiuka.
Awali Mhifadhi Mkuu wa KINAPA, Erastus Lufungulo, alisema moto
uliobainika Jumapili iliyopita, umeteketeza eneo la hekari 40 na kwamba
juhudi za kuudhibiti zilizaa matunda baada ya kupata msaada wa askari
mgambo kutoka wilaya zote mkoani hapa
Na Dixon Busagaga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni