Kwa wananchi wa Uganda, jina la Denzel Mwiyeretsi siyo geni kwa
kuwa ni mtangazaji wa masuala ya mjini katika Kituo cha Televisheni cha
XFM, lakini Denzel pia ni maarufu kwa wafuatiliaji wa Big Brother
kutokana na kushiriki shindano hilo nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, watu wengi wanamfahamu kwa mitindo ya uvaaji wake wa suruali za kubana.
“Mitindo ni kama umri, haiwezi kuwa vilevile. Ni
kama vile mvinyo mtamu, pamoja na umri, mtindo wako lazima uwe na
mwonekano mzuri. Ni kujaribu kitu kipya. Mimi ni mtu mwenye kuthubutu na
napenda kujaribu vitu vipya (ikiwamo mitindo) ili kufanya maisha yangu
yawe yenye mvuto,” alisema Denzel.
Pamoja na tabia yake ya kupenda kuvaa suruali za
kubana kuna watu akiwamo dada yake hakupendezwa na hali hiyo, siku moja
dada yake alimwambia hapendezwi na uvaaji huo.
“Miaka miwili iliyopita, dada yangu aliniambia
kuwa uvaaji wangu wa suruali za kubana unaweza kuwafanya watu wanihisi
mimi ni ‘shoga’. Lakini nilimueleza uvaaji huo ni mtindo wa maisha
yangu,” alisema Denzel aliponukuliwa na gazeti la New Vision la Uganda.
Ingawa dada yake anauona uvaaji wake unalingana na
wanaume wenye vitendo vya ushoga, aliendelea kutetea kuwa mpenzi wake
wa kike amekuwa akimsifia kwa uvaaji wake wa suruali za mtindo wa
kubana.
Hata hivyo, siyo watu wa kawaida pekee ndiyo wenye
kukwazwa na mtindo wa uvaaji wa nguo za kubana wa Denzel. Hata
madaktari nao wametoa ushauri wao kuwa uvaaji wa suruali za kubana ni
hatari kiafya
.
Lakini hoja za madaktari hazionyeshi kumteteresha
Denzel ambaye alijibu kwa kusema kuwa ni madaktari hao hao wanaosema
kunywa maji kwa kutumia vyombo vya planstiki ni hatari. Je? tumeacha
kunywa maji kwenye chupa za plastiki? Kila tunachofanya ni hatari. Kitu
kizuri ni kwamba sijawahi kuugua kwa sababu ya uvaaji wa mtindo wangu wa
suruali za kubana.”
Mchambuzi wa masuala ya mitindo, Keturah Kamugasa
alisema suruali za kubana ni mtindo wa zamani ambao umerudi kwa kasi,
hasa kupitia suruali aina ya jinsi. “Zamani zilikuwa zikiitwa ‘bomba’.”
Suruali za kubana mwanzoni zilivaliwa na wanasiasa
wa kundi la mlengo wa kushoto la Sans-culottes, ambao walikuwa
wapinzani wakubwa wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa, wakati huo suruali
hizo waliziita ‘pantaloons’.
Uvaaji huo ulianza kama uasi na kuwa mtindo wenye
umaarufu katika miaka ya 1950. Suruali hizo baadaye zikaanza kuvaliwa na
mastaa wa rock’n’roll katika miaka ya 1960 na kuendelea kusambaa katika
jamii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni