Imebainika kuwa baadhi ya madereva wa pikipiki maarufu kama
bodaboda wanatumia usafiri huo kuwarubuni na kuwashawishi wanafunzi wa
kike wa shule za msingi na sekondari na kufanya nao ngono.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili jijini
Dar es Salaam katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondononi, umebaini
kuwa wanafunzi wengi wamejiingiza katika vitendo vya ngono baada ya
kunaswa na ulaghai wa madreva bodaboda wengi wakiwa vijana wadogo.
Madereva hao wamekuwa wakifanya ngono na
wanafunzi, baada ya kuahidi kuwasafirisha bure kwenda na kurudi kutoka
shuleni, hasa kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa daladala au eneo
lililo mbali na kituo cha basi wakati wa kutoka au kwenda shuleni.
Gazeti hili limebaini kwamba, baadhi ya walimu pia
wamejiingiza katika mchezo huo mchafu na kufanya ngono na vijana wadogo
wanaoendesha bodaboda.
Madereva hao wanaoonekana katika vituo vya
daladala, huwafuata wanafunzi hao wanaosumbuliwa na shida ya usafiri
wakikataliwa kupanda daladala makondakta wa daladala hasa wakati wa
asubuhi na jioni.
“Njoo asubuhi utaona wanafunzi wanavyohangaika
kupata usafiri, mtu amefika kituoni toka saa kumi na mbili hadi saa
mbili bado yupo hapa kila basi linalokuja anaambiwa wanafunzi wametosha.
Katika mazingira haya kwanini asirubuniwe na mtu wa bodaboda?” alihoji
mmoja wa wazazi alijitambulisha kwa jina la Mwambene na kuongeza:
“Kuna baadhi ya madereva ninawafahamu wana
uhusiano na wanafunzi wawili hadi watatu, tena hawachagui mwanafunzi wa
shule ya msingi au sekondari, lazima wazazi wawafuatilie watoto wao
vinginevyo wanafunzi hawatamaliza masomo.”
Baadhi ya madereva bodaboda walisimulia
wanavyowashawishi na kuwanasa wanafunzi, wakikiri kulitumia tatizo la
usafiri wa kwenda na kurudi kutoka shuleni kuwapata kirahisi wanafunzi.
Akionekana kuvifurahia vitendo hivyo, mmoja wa
madereva wa bodaboda katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho, (jina
tunalo) alisema baadhi ya wanafunzi wanaona ufahari kupelekwa shuleni
kwa pikipiki jambo linalowafanya wawe tayari kukubali kufanya ngono.
“Wapo wanafunzi wanaopenda kuonekana wanatoka
katika familia bora, ...hao ndiyo rahisi sana kuwapata, ukimpeleka
shuleni mara ya kwanza, mara ya pili basi umemaliza mchezo,” alisema
dereva huyo akijinasibu.
Alisema baadhi ya wanafunzi hutoka nyumbani kwao
wakiaga wanakwenda shuleni lakini badala yake hukutana na madereva wa
bodaboda ambao huwapeleka mafichoni na kufanya nao ngono
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni