Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
Polisi kadhaa wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa lengo la
kumkamata.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mbowe
mwenyewe zinaeleza kuwa askari hao waliokuwa na silaha walivamia nyumba
hiyo iliyopo eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia
jana wakiwa na silaha.
Mbowe alisema hata hivyo walikwama kumkamata, kwa sababu alikuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za chama.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikataa kuzungumzia
zaidi suala hilo akieleza kuwa anayeweza kulizungumzia zaidi ni Ofisa
Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni,
Camillius Wambura alipoulizwa alisema kuwa hana taarifa za polisi
kumtafuta Mbowe.
“Sina taarifa polisi wangu kumtafuta Mbowe,” alisema Wambura.
Lakini Ofisa Habari wa Chadema Tumaini Makene
aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa askari hao walifika nyumbani kwa
Mbowe saa 7:16 usiku, wakidai kuwa na hati ya kumkamata Mbowe kutokana
na makosa ambayo hata hivyo hawakuyabainisha.
“Ni kweli askari walifika nyumbani kwa Mwenyekiti
wakidai walikuwa wakihitaji kumkamata. Kinachotushangaza ni kwamba mtu
ambaye anafahamika na wanajua ni mbunge na kiongozi wa chama, lakini
wanakwenda kumkamata kama jambazi, usiku wa manane,” alisema Makene.
Alisema kuwa polisi hao walifika nyumbani kwa
Mbowe na kukutana na walinzi katika nyumba hiyo, waliowaeleza kuwa
mwenyekiti huyo wa Chadema alikuwa safarini.
Makene hakuwataja majina walinzi waliokutwa ,
lakini nalisisitiza kwamba polisi hao waliacha namba za simu kwa walinzi
hao, wakitoa maelezo kuwa pindi Mbowe atakaporejea wamwarifu na
kuwapigia polisi kwa kuwa alikuwa akihitajika kituoni.
Ofisa huyo alieleza kuwa wakati wa tukio hilo
Mbowe hakuwapo nyumbani na alikuwa safarini mkoani Kilimanjaro,
kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Hai.
Makene alisema wanashangazwa na vitendo vya Polisi
kusaka viongozi wao usiku wa manane kama majambazi sugu, wakati
wakifahamika ni wabunge.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni