Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kunasa
waraka wa siri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaokwenda kwa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, ukimshinikiza
kukubali mapendekezo yao.
Waraka huo wa CCM uliosainiwa na Mbunge wa Jimbo
la Babati Vijijini, Jitu Vrajilal Soni una lengo la kupinga mapendekezo
mbalimbali yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya
iliyozinduliwa Juni 3 mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki na Pwani,
Mabere Marando akihutubia mkutano wa chama hicho uliofanyika katika
viwanja cha Shule ya Msingi Ukombozi, Manzese jijini jana alidai waraka
huo una lengo la kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya yenye manufaa
kwa Watanzania wote.
Marando akisoma baadhi ya mapendekezo ya CCM
yaliyomo katika waraka huo kwenda kwa Jaji Warioba kumtaka kuviondoa
vipengele vilivyomo ndani ya Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya
vinavyohusu Tunu ya Taifa, kuwa bila kufanya hivyo hakutakuwa na tija ya
uwajibikaji.
Alizitaja tunu hizo za taifa kuwa ni kuwa utu,
uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa ambazo
Chadema wanaziunga mkono zipite na kuwa sheria.
“Sisi Chadema tunaona zinafaa kutokana na umuhimu
wake lakini CCM wamemwambia Warioba aondoe neno uwazi wakiwa na maana ya
kuwa wanataka mambo yao yasiwekwe wazi,” alisema Marando.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya
chama hicho alisema, Jaji Warioba amependekeza utajiri wa taifa
uendelezwe na kuzuia mtu kumnyonya mwenzake jambo ambalo CCM
wamelipinga.
“CCM katika waraka huo ibara ya 11.2 na 11.3
wamemwambia Warioba viondolewe, sasa viongozi wa CCM na Chadema ni kina
nani wanawapenda wananchi wake,” aliwauliza wananchi waliojitokeza
katika mkutano huo na kujibiwa na kelele kuwa ni Chadema.
Marando alisema katika kipengele cha maadili ya
taifa na jamii kinachosema viongozi wanatakiwa kuzingatia uongozi,
utoaji wa huduma, kufanya usawa na kupiga vita rushwa mapendekezo ambayo
yakipita kuwa sheria yatasaidia kupunguza tatizo la rushwa la utoaji wa
huduma uliotukuta.
“CCM ambao hawaonyeshi dhamira ya kumkomboa
mwananchi wake, wamemwambia Warioba kuyaondoa maadili hayo kwani
hayafai, sasa kupiga watu, kula rushwa kweli liondolewe? Hawa CCM kweli
hawataki tupate katiba ya kuwakomboa wananchi,” alisema Marando na
kuongeza:
“Kama hiyo haitoshi wamesema kitendo cha wananchi
kumwajibisha mbunge wao kama hatakuwa anatimiza majukumu yake nao
wamesema mapendekezo hayo hayafai. Kweli CCM hawataki tupate Katiba
Mpya.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni