SUALA la Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, kusimamishwa masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), limetua bungeni baada ya baadhi ya wabunge kuitaka Serikali kuifuta sheria inayoruhusu mwanafunzi kusimamishwa masomo.
Uongozi wa chuo hicho ulimsimamisha masomo Nondo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu, baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakima Mkazi Mkoa wa Iringa.
Nondo alisimamishwa Machi 26, mwaka huu kwa barua aliyoandikiwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye.
Kutokana na hali hiyo Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), aliitaka Serikali kufuta sheria hiyo kwa kuwa inakiuka haki za binadamu.
Bobali alitoa kauli hiyo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyowasilishwa juzi na Profesa Joyce Ndalichako.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa chuo kikuu anasimamishwa masomo baada ya kushtakiwa kwa sababu tu kanuni za uongozaji wa chuo (prospectus) zinazuia mwanafunzi husika asiendelee na chuo.
“Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri, watanzania wote wana haki ya kushtaki au kushtakiwa isipokuwa rais wa Tanzania, lakini elimu ya chuo kikuu ni elimu ya ngazi ya tatu.
“Mwanafunzi huyu amepita elimu ya msingi na sekondari hadi kufikia elimu ya chuo kikuu, wanaosoma pale siyo lazima wawe vijana hata watu wazima wanasoma na wapo wengine wanaoshtakiwa.
“Sasa jambo la Nondo kuwa ameshtakiwa na kusimamishwa masomo, kama kuna sheria ya kanuni za uongozaji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zinasema hivyo, muongozo wa namna hiyo haufai.
“Sheria hiyo inafaa ifutwe kwa sababu haiendani na wakati kwa sababu inanyima na kuzuia haki za binadamu lakini pia inakwenda kinyume na katiba ya nchi inayotoa fursa ya mtu kushtaki na kushtakiwa.
“Nasema kwa sababu najiuliza ni kweli kati ya wanafunzi wote waliopo vyuo vikuu aliye na kesi mahakamani ni Abdul Nondo pekee? Ni kweli?
“Kama sheria za chuo zinasema hivyo nakushauri waziri zifuteni zinawatia aibu vinginevyo mtuambie jambo hili mnalichukualia kisiasa,” alisema Bobali na kukatizwa na taarifa iliyoombwa na Mbunge wa Mgogoni (CUF), Dk. Ally Yusuf Suleiman.
Dk. Yusuf alisema: “Kama alivyosema mchangiaji kwamba ni haki ya kushtaki na kushtakiwa na bila ya kupoteza nafasi tunao wabunge wameshtakiwa mahakamani na wengine wamefungwa lakini hawajapoteza ubunge wao. Inakuwaje mwanafunzi huyu ambaye kashtakiwa tena kwa makosa ya kubambikiziwa kwa kuwa hayajathibitishwa… inakuwaje afutwe masomo?”
Hata hivyo, Mbunge huyo alikatishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ambaye alisema huo ni mchango wake na si taarifa.
“Jambo hili linakichafua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lazima tuseme ukweli… hadhi ya UDSM kwa sasa tunataka kukiingiza kwenye siasa.
“Ukifanya sensa ya wanafunzi wangapi wenye kesi mahakamani hawatapungua wanafunzi 20 au 30 ila aliyeonekana mwenye kosa na kunyimwa kuendelea na masomo ni mmoja tu. Hii si haki kabisa,” alisema.
Mbunge wa Mgogoni (CUF), Dk. Ally Yusuf Suleiman alimtaka Waziri Ndalichako kubainisha kiwango cha fedha za mikopo ya elimu ya juu kilichotengwa kwa ajili ya wanafunzi wanaotokea Zanzibar.
Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta (CCM), aliitaka Serikali kuunda bodi huru ya usimamizi wa elimu.
“Bodi hii itaangalia mitihani inayotungwa na mambo mengine muhimu ambayo yanaweza kuboresha elimu yetu.
Mbunge wa Kuteuliwa, Abdalah Bulembo aliitaka serikali kueleza imejiandaaje kuwapokea wanafunzi watakaohitimu darasa la sita na saba mwaka 2020 baada ya sera ya elimu nchini kubainisha kuwa kuanzia mwaka 2015 elimu ya msingi itakuwa miaka sita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni