Katika utafiti wakuchunguza athari za msongo wa mawazo katika moyo, madaktari Mayer Friedman na Ray Roseman waliweza kuwaweka watu katika makundi ya haiba mbili; yaani haiba kundi A and haiba kundi B.
Madaktari hawa waligundua kuwa hata kama kazi na aina ya maisha ingefanana, watu wa haiba kundi A wangekuwa na nafasi mara 3 kuteseka na msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu n.k. na watu hawa mara nyingi huwa wanamaudhi kwa jinsi wanavyojibu au kuongea na wengine, na hili limekuwa likiwaongezea msongo wa mawazo maradufu.
Makundi haya yamewekwa ili kukuwezesha wewe kujua uko upande gani. Usichanganyikiwe wala kushtuka pale utakapojikuta una tabia za makundi yote mawili, mara nyingine inaamaanisha kuwa uko vizuri katika kuhakikisha mambo yanafanyika inavyotakiwa au unavyotaka yawe. Ila kama unajikuta unatabia zaidi ya nusu za haiba kundi A inabidi uchukue uamuzi wa kutafuta kubadilika au kubalisha mtazamo ulionao katika maisha, kabla haujajihatarishia maisha yako wewe mwenyewe.
Haiba Aina ‘A’
– Ni watu wa ushindani katika kila kitu wafanyacho.
– Watu wenye haiba ya kutumia nguvu na kulazimishisha
– Hufanya mambo yao mengi kwa haraka
– Huwa na uchu wa kupandishwa vyeo na kujulikana katika jamii. (Hatakama hawana sifa).
– Hutaka sana kujulikana na kuheshimiwa kwa kile walichokifanya.
– Hukasirishwa kwa haraka na watu au matukio fulani
– Huongea mara kwa mara kwa kufoka au kwa vitisho
– Hupenda kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
– Hutembea na hata kula kwa haraka
– Mara nyingi kuchukizwa sana pale wanapocheleweshwa
– Hujali sana muda na kukazana kumaliza mambo kwa muda ulipangwa (meating deadlines)
– Kila mahali huwepo kwa wakati na kwa muda muafaka.
– Mara kwa mara misuli yao ya uso huonyesha, kumaanisha, kuogopesha au ukali,
Haiba Aina ‘B’
– Sio watu wa ushindani mfano, makazini, michezoni, masomoni n.k.
– Ni watu walio rahisi, na huyakubali mazingira, hufanya vitu taratibu na kwa kufuata kanuni.
– Huendelea na kuchukuliana na hali ya kazi iliyopo.
– Huridhika na nafasi walinayo katika kijamii.
– Hawahitaji kujulikana au kutambulika katika jamii au hata katika matukio.
– Sio rahisi sana kuwaudhi.
– Mara nyingi hufurahia sana wanapokuwa pekeyao.
– Ni wavumilivu.
– Hupendelea kufanyakitu kimoja kwa muda muafaka kabla ya kwenda kwenye kitu kingine.
– Hutembea, na kula kwa nafasi na utulivu.
– Hawakimbizwi sana na muda, sio wakukimbizana sana na kumaliza kazi.
– Mara nyingi ni wachelewaji.
– Nyuso zao ni za kufurahi na sio za mikunjo.
KWANINI UKO VILE ULIVYO?
Vyovyote haiba yako ilivyo na kwa vyovyote unavyowachukulia wale wenye tabia ngumu fahamu kuwa mfano huo ulishakuwepo miaka mingi iliyopita, labda zaidi ukiwa mtoto ndio ilikuwa chanzo cha vile ulivyo leo; Mwanasaikolojia mmoja aliuita mfumo huu “A child is a father of a man” yaani
Mambo tunayoyaona au unayoyaona kwa mtoto hutupa picha halisi ya ukumbwa wake utakavyokuwa. Zaidi ya asilimia sitini ya yote yanayoendelea maishani mwetu leo yanachangiwa na makuzi yetu tukiwa watoto. Wengi wetu tumejiharibia misingi yetu ya uwezo wa kuishi na watu wenye tabia ngumu na hivyo kujikuta tunaumizwa tokea tukiwa watoto wadodo. Habari njema ni kwamba hakuna ulazima wa kubaki vile ulivyo, mabadilko yanawezakana, inawekana katika hatua yoyote kubadili mtazamo au muonekano wako na kuboresha ujasiri wako.
Tujaribu kuangalia baadhi ya sababu zinazosababisha mtu kujiona au kujitazama vibaya, hii itakuwezesha wewe kujua uko wapi na kwanini.
1. Watu wa kwanza kabisa waliowahi kuwa karibu na wewe ni baba na mama yako au yoyote aliyechukua nafasi yao, mfano mlezi, babu, bibi nk. Kutokana na mtazamo wao juu yako, hapo wewe umetengeneza au kuzalisha mtazamo juu yako mwenywe najinsi unavyojithamini au kutojithamini. Kwa lugha rahisi ni kwamba, jinsi unavyojiangalia ulivyo leo kunatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi wao walivyokuwa wanakutazama, kama walikuona wewe lofa na mjinga basi kuna uwezekano mkubwa na wewe leo utajiona lofa tu.
Najua wapo wazazi wasio na hekima wala wema kwa watoto wao, huwasababishia watoto wao majeraha ya kimwili, kihisia na hata kiakili, uzuri ni kwamba fungu la wazazi hawa ni dogo. Ingawa inawezekana sana kwa wazazi au walezi au watu wazima wowote kusababisha majeraha na athari kwa watoto mara nyingine pasipo kujua kwamba wanafanya hivyo. Katika kuongea na wazazi lukuki nimegundua kwamba asilimia kubwa ya watoto wameharibiwa na wazazi wao wenyewe, pasipo wazazi hawa kujua kuwa wanawaharibu watoto wao.
2. Wazazi ambao huwalinda na kuwatetea sana watoto wao, wakijaribu kuwafanyia kila kitu kwa niaba ya watoto hao, kwa njia hii wazazi hawa hutengeneza watu wazima (wababa au wamama) wenye utegemezi mkubwa, wasioweza kufanya kitu chochote wenyewe wala kusimama kwa miguu yao wenyewe. Unakuta hata kazi za shuleni mama ndiyo anafanya, mtoto anakuwa hata kuosha mwili wake hajui, na hawa ndio wale ambao ndoa huwashinda mapemaaa.
3. Wale wazazi au walezi ambao hutoa mahitaji kwa watoto wao lakini hushindwa kuonyesha kwa matendo upendo wao kwa watoto wao (mfano. Kuongea nao, kucheka nao, kucheza nao n.k.) hutengeneza kizazi kinachoamini kuwa hakipendeki, hakina mvuto, kisicho na thamani na kisichostahili kupendwa. Baba haijalishi unatoa mahitaji yote yanayohitajika nyumbani kwako, hilo sio pekee watoto wako wanalolihitaji kutoka kwako, wape muda wakuwa pamoja nao, waruhuru kucheza na wewe kidogo, toka pamoja nao, jibu baadhi ya maswali yao, waruhusu kujuwa kumbe baba au mama anaweza kuwakaribu na sisi pia.
4. Wazazi au walezi ambao kila mara humwekea mazingia mtoto kujiona aliyeshindwa, kila wakati ni wakufeli tu, wazazi hawa ni wale wanaosema kwa nini mtoto asijitahidi, kwanini asiwe wa kwanza darasani, ni mpumbavu n.k.. hali hii huharibu kabisa imani ya mtoto kwake yeye mwenyewe, huua kule kujiamini kwake na pia kutokiamini kile anachokifanya.
Yawezekana kuna vitu vilivyoonekana katika makuzi ya mtoto ambavyo hakuna wa kulaumiwa lakini bado vitu hivi huathiri sana kujiamini na kujithamini kwa mtoto yule.
Mtoto au watoto wanaohama hama au kuhamishwa shule mara kwa mara, kwa sababu zao binafsi au kwa sababu ya kuhama hama kwa wazazi hupata shida yakujiona wapweke kwa maana kila wakati hupata kazi ya kutengeneza marafiki wapya na kwamuda fulani hali hii huathiri haiba zao na kujenga kitu tunachokiita “inferiority complex”