Ben Paul
Wakati wasanii wengine wakifanya
juhudi kuhakikisha wanasafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya
kutengeneza video za nyimbo zao,, mwimbaji mwenye sauti ya kuvutia,
Bernard Paul maarufu ‘Ben Pol’ amesema kuwa hana mpango wa kutengeneza
video nje ya Tanzania.
Ben Pol amesema licha ya video zake nyingi kuwa
amezifanyia hapa nchini, lakini zimefanikiwa kuonyeshwa katika vituo
mbalimbali vya televisheni Afrika Kusini na Afrika Mashariki kwa jumla.
“Iwapo nitataka kutengeneza video kali ya
kimataifa, nitamchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta hapa Tanzania,”
hivi ndivyo anavyosema.
Anasema kuwa ndani ya Tanzania kuna vivutio vingi
anavyoamini akimchukua mwongozaji mwenye vifaa vya kutosha vya
kimataifa, ataweza kutengeneza video yenye ubora.
“Unapomchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta
hapa, bila shaka itampa umakini mkubwa hata yeye mwenyewe, hivyo kufanya
mambo makubwa zaidi ya afanyavyo akiwa huko. Hapa kwetu tuna vivutio
vingi , maeneo yanayovutia kuna Lushoto, Arusha, Zanzibar, Bagamoyo na
mengine yanayoweza kutumika kwa shughuli hii na ukaushangaza ulimwengu,”
anasema Ben Pol.
Anasema kuwa bado anahisi anao wajibu wa kuutangaza utalii wa ndani kupitia kazi yake ya muziki.
“Nina wajibu na jukumu la kuwa balozi mzuri
nyumbani kwetu. Najua labda watu wa nje wangependa kuona vitu vya
nyumbani, ninapojitangaza kwamba mimi ni mwanamuziki kutoka Tanzania,
hata kwenye kazi zangu waone mazingira ya nchi yangu,” anasema.
Je, hiyo ni sababu pekee ya uamuzi wake kufanyia kazi zake Bongo?
Ben Pol anaeleza kuwa, anapoona kazi zake
zinatumika na kuombwa na watu wengi waishio nje ya nchi, hufarijika
kwani inaonyesha inaeleweka.
“Najua kazi yangu inaeleweka, kwa watu wanaoijua
lugha ninayoimba, hata kwa wale ambao Kiswahili kwao ni mtihani. Napokea
pongezi nyingi, mfano wimbo wa ‘Jikubali’ ni kati ya kazi zangu
zilizonipa umaarufu mkubwa nje ya nchi na ndiyo wimbo uliopigwa zaidi
nje kuliko kazi zangu zote,” anasema Ben Pol.
Kuhusu usimamizi wa kazi zake Ben Pol anasema kuwa
kwa sasa kuna mtu wa karibu anayemsaidia katika suala hilo. Anamtaja
kuwa ni mshirika wake wa karibu na wanasaidiana katika kazi za muziki,
lakini hana meneja.
Anabainisha kuwa kuna faida kubwa kwa msanii kuwa
na usimamizi, lakini akasema bado kuna uhaba wa mameneja wa kazi za
wasanii na kwamba kwa walipo sasa, wengi hawana ufahamu wa kazi zao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni