Jumanne, 26 Agosti 2014
Jumamosi, 23 Agosti 2014
BEN POL: SIHITAJI KWENDA NJE YA NCHI
Ben Paul
Wakati wasanii wengine wakifanya juhudi kuhakikisha wanasafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza video za nyimbo zao,, mwimbaji mwenye sauti ya kuvutia, Bernard Paul maarufu ‘Ben Pol’ amesema kuwa hana mpango wa kutengeneza video nje ya Tanzania.
Ben Pol amesema licha ya video zake nyingi kuwa amezifanyia hapa nchini, lakini zimefanikiwa kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni Afrika Kusini na Afrika Mashariki kwa jumla.
“Iwapo nitataka kutengeneza video kali ya kimataifa, nitamchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta hapa Tanzania,” hivi ndivyo anavyosema.
Anasema kuwa ndani ya Tanzania kuna vivutio vingi anavyoamini akimchukua mwongozaji mwenye vifaa vya kutosha vya kimataifa, ataweza kutengeneza video yenye ubora.
“Unapomchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta hapa, bila shaka itampa umakini mkubwa hata yeye mwenyewe, hivyo kufanya mambo makubwa zaidi ya afanyavyo akiwa huko. Hapa kwetu tuna vivutio vingi , maeneo yanayovutia kuna Lushoto, Arusha, Zanzibar, Bagamoyo na mengine yanayoweza kutumika kwa shughuli hii na ukaushangaza ulimwengu,” anasema Ben Pol.
Anasema kuwa bado anahisi anao wajibu wa kuutangaza utalii wa ndani kupitia kazi yake ya muziki.
“Nina wajibu na jukumu la kuwa balozi mzuri nyumbani kwetu. Najua labda watu wa nje wangependa kuona vitu vya nyumbani, ninapojitangaza kwamba mimi ni mwanamuziki kutoka Tanzania, hata kwenye kazi zangu waone mazingira ya nchi yangu,” anasema.
Je, hiyo ni sababu pekee ya uamuzi wake kufanyia kazi zake Bongo?
Ben Pol anaeleza kuwa, anapoona kazi zake zinatumika na kuombwa na watu wengi waishio nje ya nchi, hufarijika kwani inaonyesha inaeleweka.
“Najua kazi yangu inaeleweka, kwa watu wanaoijua lugha ninayoimba, hata kwa wale ambao Kiswahili kwao ni mtihani. Napokea pongezi nyingi, mfano wimbo wa ‘Jikubali’ ni kati ya kazi zangu zilizonipa umaarufu mkubwa nje ya nchi na ndiyo wimbo uliopigwa zaidi nje kuliko kazi zangu zote,” anasema Ben Pol.
Kuhusu usimamizi wa kazi zake Ben Pol anasema kuwa kwa sasa kuna mtu wa karibu anayemsaidia katika suala hilo. Anamtaja kuwa ni mshirika wake wa karibu na wanasaidiana katika kazi za muziki, lakini hana meneja.
Anabainisha kuwa kuna faida kubwa kwa msanii kuwa na usimamizi, lakini akasema bado kuna uhaba wa mameneja wa kazi za wasanii na kwamba kwa walipo sasa, wengi hawana ufahamu wa kazi zao.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)